Msukumo wa ndani na motisha huamua uwezo wetu wa kufikia malengo. Kusimamia matatizo yaliyopo na kufanya mambo kwa kuzingatia mapendeleo yetu ya msingi kunaweza kusaidia.
Je, ni lengo gani kubwa zaidi ulilowahi kulifikia? Watu wengine hujibu swali hili bila kukawia. Wanaweza wakajibu kwamba walihitimu shahada ya chuo kikuu, walimlea mtoto, au walinunua nyumba. Mifano mingine inaweza isiwe dhahiri sana, lakini inaweza kujumuisha mambo kama kumaliza mbio za masafa marefu ya ndani, kujifunza kucheza ala ya muziki, au kuishinda changamoto fulani ya maisha kama vile ugonjwa au jeraha.
Hakuna shughuli au lengo lolote miongoni mwa haya lililo rahisi. Watu hawayafikii malengo haya kwa kuishi tu kiholela kila siku na kusubiri kuona kile kitakachotokea. Kulifikia lengo huhitaji shauku au hitaji, udumifu, udadisi, ushupavu, na motisha. Utayari na uwezo wa kukamilisha hatua zinazopelekea malengo haya hutengeneza msukumo wa ndani na motisha yetu.
Msukumo wa ndani na motisha ni mojawapo ya vipengele (kategoria) vidogo vinavyopimwa katika kipimo cha MHQ cha Milioni ya Afya ya Akili (Kiwango cha Afya ya Akili). Kuwa na msukumo wa ndani wenye afya na motisha humaanisha kuwa una uwezo wa:
- Kuanzisha na kuvumilia kazi na shughuli ngumu hadi zitakapokamilika
- Kuwa mdadisi, kupendezwa, kuchangamkia, na kuwa na shauku kuhusiana na ulimwengu unaokuzunguka
- Kushinda changamoto na vikengeusha fikra vinavyokuzuia kufikia malengo yako
Sote tuna shughuli maishani ambazo hatujazikamilisha kutokana na sababu moja au nyingine. Lakini ikiwa una tatizo sugu la kutokamilisha malengo na miradi, unaweza ukawa unakabiliana na tatizo la kiwango kidogo cha msukumo wa ndani na motisha. Katika hali hii, baadhi ya matatizo yafuatayo yanaweza kuvuruga msukumo wa ndani na motisha:
- Hali binafsi (kama vile matatizo binafsi nyumbani, au matatizo ya umma katika jamii au eneo lako)
- Maumivu ya hivi karibuni au yaliyokwisha kupita yanayokusababishia huzuni au ukengeufu wa fikra
- Masuala ya afya ya kimwili ambayo husababisha ukengeufu wa fikra au kukata tamaa
- Uraibu unaotawala namna unavyotumia muda wako, kama vile matatizo ya kutumia madawa, michezo ya video, au kucheza kamari
Utatuzi wa Matatizo
Ikiwa unataabika katika msukumo wa ndani na motisha, kubainisha kinachoendelea na jinsi unavyoweza kupata usaidizi au kujisaidia mwenyewe kunaweza kukusaidia. Kwa mfano, watu wengi wenye matatizo ya unyogovu huwa na kiwango cha chini cha msukumo wa ndani. Mojawapo ya maswali ambayo wataalamu wa tiba huwauliza sana wateja ni hamu yao ya vitu walivyokuwa wakifurahia awali kama imepungua. Kuzungumza na daktari au mtaalamu wa tiba kuhusiana na hisia hizi kunaweza kusaidia kujua nini kinachoendelea. Kisha unaweza kuanza kushughulikia suala hilo.
Kutunza maeneo mengine ya ustawi wa afya kunaweza pia kusaidia kutatua tatizo la msukumo wa ndani na motisha. Hisia na mtazamo wa kifikra pamoja na uhusiano wa akili-mwili vyote vina uhusiano wa wazi katika msukumo wa ndani na motisha, kwa mfano.
Ikiwa una alama hasi za MHQ kwenye msukumo wa ndani au motisha, unapaswa kuwasiliana na daktari au mshauri mwenye sifa. Mtaalamu anaweza kukusaidia kutathmini hali hiyo na kugundua nini kinachoendelea. Nchini Marekani, unaweza kuwasiliana na Idara ya Huduma za Afya ya Akili na Udhibiti wa Matumizi Mabaya ya Dawa. Ikiwa una mawazo ya kufanya vurugu au ya kutaka kujiua, unapaswa kuwasiliana na huduma za dharura zilizopo katika eneo lako, pamoja na daktari au mtaalamu wa tiba, na kutembelea vituo vya Kuzuia Vitendo vya Kujiua ili kupata msaada.
Tazama chapisho linalohusiana: MHQ hasi ni ishara inayokutaka kutafuta msaada wa matibabu.
Kuongeza Msukumo wa Ndani na Motisha
Ikiwa unatafuta tu kudumisha au kuboresha msukumo wako wa ndani na motisha, basi ushauri hupatikana tele. Sehemu kubwa ya tasnia ya kujisaidia mwenyewe na kupata mafunzo, imejengwa katika nadharia hii.
Utafiti mwingi umejizatiti katika umuhimu wa motisha ya ndani (kutoka ndani ya mtu) na ile ya nje (kutoka nje ya mtu). Kwa mujibu wa watafiti wawili wa saikolojia chanya (Stefano Di Domenico na Richard Ryan), watu wanaohamasishwa kutoka ndani “hushiriki katika shughuli kutokana na kuiona kuwa ya kupendeza na ya kuridhisha.” Watu wanapohamasishwa na mambo ya nje, hukamilisha shughuli kutokana na kutaka “kupata zawadi, kuepuka adhabu, au kupata matokeo yenye thamani fulani.”
Kwa mfano, Sandra anaweza kuwa na motisha ya ndani ya kujifunza lugha mpya kwa sababu anapenda isimu, lakini akawa na motisha ya nje ya kufanya kazi asiyoipenda kutokana na kuhitaji kulipa bili zinazomkabili. Wataalamu wengi hukubali kwamba sote huhitaji motisha ya ndani na motisha ya nje ili kufanikiwa katika malengo yetu maishani, ingawa wengine huamini kuwa motisha za ndani ndizo zidumuzo.
Ikiwa unataka kuongeza motisha yako ya ndani kwa kazi unazoziona kuwa za kuchosha, unaweza kufikiria kujaribu kwa muda mfupi, kazi zisizotamanika sana kwa ajili ya malengo ya muda mrefu. Kwa mfano, kwenda kazini kila siku katika ajira usiyoitaka kunaweza kukusaidia kupata pendekezo zuri la kazi bora zaidi hapo baadae. Kukumbuka hili wakati unapojihisi kuchoshwa au kukata tamaa kazini kunaweza kukusaidia. Vile vile, kupata alama ya kufaulu katika kozi ya elimu ya jumla kama vile Aljebra kunaweza kukusaidia kumaliza shahada ya historia iliyo muhimu kwako, hata kama darasa la Aljebra linaonekana kutohusiana kabisa.
Sisi sote hukabiliana na tatizo la msukumo wa ndani na motisha mara kwa mara. Kukengeushwa kifikra ama kubadilisha mwelekeo mara moja moja ni kawaida. Ikiwa wewe hupitia shida hii mara kwa mara zaidi, na ungependa kuongeza alama yako ya MHQ, basi kushughulikia masuala ya ustawi wa afya yaliyopo na kutambua motisha zako za ndani kunaweza kusaidia.