Jinsi tunavyoshughulikia hisia na vikwazo huathiri ustawi na mtazamo wetu wa maisha kiujumla.
Sote tumekutana au kushuhudia watu ambao kamwe hawaonekani kuvunjika moyo. Haijalishi ni mambo gani ya kutisha yamewapata, wao huendelea kufuata malengo yao, bila kuyumbishwa. Ingawa wanaweza kuwa wanapitia ugumu zaidi nyuma ya pazia kuliko tunavyotambua, wanaweza pia kuwa na uthabiti wa asili unaowafanya wasonge mbele.
Sisi sote huwa na mabadiliko ya mhemko mara kwa mara. Wakati wa siku, kuhisi njaa au uchovu, au kutoelewana na rafiki kunaweza kuathiri jinsi tunavyohisi. Hali yetu ya jumla huchangiwa na jinsi tunavyodhibiti matukio haya madogo na makubwa maishani, na hisia zinazohusiana na zinazofuatana nazo. Mtazamo wetu juu ya maisha pia umefungwa katika hisia zetu, na huathiri jinsi tunavyoziona siku zijazo, na jinsi tunavyohisi kuhusu ulimwengu kwa ujumla.
Kwa pamoja, haya huunda kitengo kidogo cha hisia na mtazamo wa kifikra kwenye kipimo cha MHQ cha Milioni ya Afya ya Akili (Kiwango cha Afya ya Akili). Ingawa kuwa na hisia ni jambo la kawaida na lenye afya, huwa rahisi zaidi kwa baadhi ya watu kudhibiti hisia na tabia zao kuliko watu wengine. Watu walio na alama nzuri ya hisia na mtazamo wa kifikra katika kipimo cha MHQ, huweza kufanya yafuatayo:
- Kudhibiti tabia na miitikio yao hata wakati wa kuhisi hisia kali, na hujibu kwa utulivu wanapopitia hali za mfadhaisho.
- Kuwa na matumaini na kutengeneza maana chanya kutoka kwenye hali za kukatisha tamaa, au kugeuza uvunjwaji moyo kuwa hali chanya zaidi.
- Kuinuka tena baada ya kupitia vikwazo.
Wale walio na alama ya chini ya hisia na mtazamo wa kifikra wanaweza:
- Kupata hofu ya mara kwa mara, mfadhaiko, wasiwasi, au taharuki.
- Kupata ugumu wa kudhibiti hisia zao na mara kwa mara kuhisi kulemewa nazo.
- Kuwa na dalili za mara kwa mara za kimwili kama vile matatizo ya tumbo, au kuwa na matatizo ya kimwili kama magonjwa ya mara kwa mara bila sababu dhahiri.
- Kujilaumu kwa mambo ambayo si makosa yao.
Athari kwenye Hisia na Mtazamo wa Kifikra
Idadi yoyote ya mambo inaweza kuathiri hisia na mtazamo wetu wa kifikra. Mambo ya kibaolojia na kinasaba, haiba zetu kuu, mahusiano na familia au wenzetu, mazingira tunayoishi, mambo tunayoyapitia maishani, na matukio ya sasa ya ulimwengu, yote huchangia.
Jinsi tunavyoshughulikia hisia, na jinsi tunavyoutazama ulimwengu, huathiri kila eneo lingine la maisha yetu. Ikiwa unahisi kuvunjika moyo kila wakati, utakuwa na uwezekano mdogo wa kufuata au hata kuwa na malengo ya maisha. Ikiwa wewe hupata ugumu wa mara katika kudhibiti hisia, unaweza kuharibu mahusiano yako au kuwa na shida ya kusimamia majukumu. Kuhisi kufadhaishwa kila wakati kunaweza pia kukufanya uwe hatarini zaidi kupata masaibu katika hali za afya ya mwili.
Vinginevyo, kuwa na uwezo wa kustahimili misukosuko ya maisha huonyesha uthabiti. Hata wakati wa kuangushwa, wale walio na ustahimilivu wa hali ya juu huweza kuinuka tena, kujaribu tena, na kuweka malengo mapya. Hata matukio mabaya yanaweza pia kusababisha shauku jipya la maisha, moyo wa shukrani, na kuyaona maisha kuwa na maana zaidi.
Je, Ninaweza Kubadilisha Alama Yangu?
Kwa bahati nzuri, hisia na mtazamo wa kifikra ni eneo ambalo tunaweza kulifanyia kazi ili kulibadilisha. Ikiwa una alama ya juu na ungependa kuidumisha hapo, endelea kufanya shughuli za kujijali. Dumisha usaidizi wako wa kijamii, hata kama utalazimika kuufanya kwa mbali, na tunza maeneo mengine ya ustawi wa afya.
Ili kudumisha au kuongeza alama ya hisia na mtazamo wa kifikra, fikiria kujaribu shughuli mpya, au kufufua mambo ya zamani yanayokuvutia ambayo hukufanya kufurahi na kuridhika. Badilisha mwenendo wako wa kimwili ikiwezekana (hata kama ikiwa ni kufanya matembezi tu mara moja kwa siku) na ujifunze kuhusu ufikiri chanya na zana za kukujengea umakini. Ushauri nasaha unaweza kusaidia katika kutambua mwelekeo wowote wa mawazo hasi na kuhoji imani hasi zinahusiana na wewe. Pia boresha au dumisha hali ya kujitunza kimwili kwa kula vizuri na kufanya mazoezi, kwenye sehemu za mazingira ya nje ikiwezekana, jambo linaloweza kuinua hisia na mtazamo wako wa kifikra. Na muhimu zaidi, pata usingizi wa kutosha.
Alama hasi katika kitengo hiki zinaweza kuonyesha kiwewe (trauma) cha zamani, masuala makubwa ya unyogovu, au hata hali ya mfumo wa neva na inaweza kuathiri taswira yako binafsi kijamii na msukumo wa ndani na motisha.
Inaweza pia kumaanisha kuwa unapitia kwenye vurugu au mawazo au tabia za kutaka kujiua. Ikiwa una mawazo ya kujiua, kujiumiza au kufanya vurugu, unapaswa kutafuta msaada mara moja. Wasiliana na daktari wako wa karibu, mtaalamu wa magonjwa ya akili au mshauri mtaalamu, na utembelee Kituo cha Kuzuia Vitendo vya Kujiua ili upate msaada.
Tazama chapisho linalohusiana: MHQ hasi ni ishara inayokutaka kutafuta msaada wa matibabu.
Hisia na mtazamo wa kifikra ni mojawapo ya vipengele muhimu vinavyoathiri maisha yetu, kwa muda mfupi na kwa muda mrefu, hutupa furaha na matumaini na kutuvisha ujasiri pindi tunapokutana na shida. Kuyapa mambo haya kipaumbele, kwa kuyadumisha au kuyaboresha, ni hatua muhimu katika kuwa na maisha chanya na yenye kufurahisha.