Blogu

Group of friends

Taswira Binafsi Kijamii ni nini?

Huu ni mtazamo wa taswira yako binafsi kijamii, maana yake, na kwa nini huwa na athari katika maisha yako.

Hebu itafakari siku ya kawaida. Unaweza kuchangamana na wanafamilia, marafiki kwenye mitandao ya kijamii, kuwa na mkutano na mkubwa wako wa kazi au mfanyakazi mwenzako, na kuzungumza na mtu ambaye ungependa kuchumbiana nae. Nyakati hizi zote, na jinsi tunavyojihisi tukiwa ndani yake, huunda taswira yetu kijamii.

Taswira binafsi kijamii humaanisha jinsi tunavyojiona katika kuhusiana na wengine. Huhusisha ujenzi wa uhusiano, uhisi wa huruma kwa wengine, na namna ya kuwasiliana. Taswira binafsi yenye afya njema au isiyo na afya njema kijamii itaathiri pia ustawi wako wa kiakili kiujumla na uwezo wa kufikia malengo ya maisha. Hii ni kwa sababu sehemu kubwa ya ulimwengu wetu ni ya kijamii na huhusisha miingiliano na wengine.

Taswira binafsi kijamii ni mojawapo ya kategoria (vipengele) zinazopimwa katika kipimo cha MHQ cha Milioni ya Afya ya Akili (Kiwango cha Afya ya Akili). Hii ni mitazamo ya baadhi ya mambo ambayo mtu mwenye taswira binafsi nzuri kijamii anaweza kupitia:

  • Hali nzuri ya kujithamini ikiwa ni pamoja na muonekano wa mwili.
  • Miunganisho na uhusiano thabiti wa kihisia na marafiki na familia.
  • Kuridhishwa na kufurahishwa na ukaribu wa kimwili katika mahusiano.
  • Uwezo wa kuwasiliana na watu kwa ufanisi na kwa namna ipasayo, kimatamshi na kwa njia isiyo ya kimatamshi.
  • Kujali na kuelewa mitazamo ya watu wengine.

Fikiria maeneo mengi ya maisha ambayo ujuzi huu unaweza kusaidia. Ikiwa unajiamini zaidi, utakuwa na uwezekano mkubwa wa kuanzisha uhusiano, kushiriki katika usaili wa ajira, au kuchukua lengo jipya la maisha. Kujisikia vizuri katika miunganisho na ukaribu wa kihisia kunaweza kuboresha mahusiano na kupunguza mfadhaiko na hisia za kutokujiamini. Huku kujiamini kunaweza pia kukusaidia kuweka mipaka, kujisimamia, na kuomba usaidizi pindi mahitaji yako yanaposhindwa kutimizwa.

Tazama chapisho linalohusiana: Kuelewa Hisia & Mtazamo wa Kifikra.

Vipi Kuhusu Alama Yangu?

Alama ya juu ya taswira binafsi kijamii kwenye kipimo cha MHQ huakisi kiasi kikubwa cha kuridhika na sisi wenyewe, na uwezo wetu wa kustawi ulimwenguni. Wale walio na alama za juu wanaweza kusalia kwenye mstari, kuwa makini kuhusiana na wao wenyewe na watu wengine, na kuendelea kuweka kipaumbele katika taswira zao binafsi kijamii.

Ili kudumisha au kuongeza alama ya taswira binafsi kijamii, endelea kujifunza kuhusu miunganisho yenye afya na ujizoeshe kuwajulia hali wengine. Ingawa fursa zinaweza kuwa chache kutokana na matakwa ya kudumisha umbali baina ya mtu na mtu ndani ya jamii, bado kuna nafasi za kuwasiliana ana kwa ana na wengine kupitia zana kama Zoom. Huduma nyingi za ndani zimerekebishwa kuendana na matukio mubashara ya mtandaoni. Kuna fursa nyingi zaidi na zaidi za kibunifu za kuchangamana na wengine. Unaweza pia kutumia nyenzo za kujisaidia, masomo na rasilimali za bure zipatikanazo mtandaoni.

Wale walio na alama za wastani au za chini za taswira binafsi kijamii wanaweza kutatizika na baadhi ya maeneo yaliyopo hapo juu, na kupitia ugumu wa kazi, changamoto katika familia na mahusiano mengine. Ushauri nasaha unaweza kukusaidia kutambua maeneo ambayo unatatizika, kupata maarifa mazuri zaidi na kujifunza njia za kuboresha taswira yako binafsi kijamii. Kwa mfano, matibabu ya kiufahamu yanaweza kukusaidia kutambua chanzo cha mawazo ambayo yanaingilia utendakazi wako wa kijamii, na kutengeneza njia mpya za kufikiria na kuchangamana na wengine. Mabadiliko madogo yanaweza kuleta tofauti kubwa.

Alama hasi katika kategoria hii ya MHQ zinaweza kuashiria masuala hatari zaidi, kama vile vitisho, tabia haribifu au za vurugu, au mawazo ya kujidhuru na kujiua. Ikiwa hii ndio hali iliyopo, unapaswa kutafuta msaada mara moja. Wasiliana na daktari wako wa ndani, mtaalamu wa tiba, na tembelea Kituo cha Kuzuia Vitendo vya Kujiua ili upatiwe msaada.

Tazama chapisho linalohusiana: MHQ hasi ni ishara inayokutaka kutafuta msaada wa matibabu.

Mitandao ya Kijamii: Inasaidia au Inadhuru?

Watu wengi hujiuliza kama mitandao ya kijamii imeathiri mitazamo yetu. Kwa kuzingatia mazingira yaliyopo, je mitandao ya kijamii ni bora kuliko njia mbadala, inayoweza kuhusisha kupunguza zaidi mwingiliano wako na wengine? Kwa kawaida, wateja katika matibabu mara nyingi hujadili mfadhaiko unaohusiana na mitandao ya kijamii, haswa katika vikundi vya vijana. Ila, huripoti pia kwamba ingelikuwa ngumu kwao kuwasiliana na wenzao kama wasingelikuwa kwenye mitandao ya kijamii.

Utafiti juu ya mada hii, uliofanywa kabla ya janga hili la UVIKO-19, una majibu yaliyochanganyika na bado huweza kujadiliwa sana. Uchambuzi mmoja wa tafiti 100+ zilizofanyika uligundua kuwa kiujumla, tovuti za mitandao ya kijamii zimeonekana kuwa na athari hasi ya wastani katika kujithamini binafsi. Hata hivyo, kulingana na waandishi wa utafiti huo, kuna uwezekano kwamba wale watu ambao tayari wana kiwango hasi cha kujithamini hutumia mitandao ya kijamii kama njia mbadala. Inaweza kuwa rahisi zaidi kwa baadhi ya watu kuwasiliana na wengine mtandaoni kuliko ana kwa ana. Pia hatufahamu bado jinsi gani athari za mitandao ya kijamii zinaweza kubadilika kutokana na mikakati iliyowekwa ya kudhibiti ukaribu baina ya mtu na mtu kwenye jamii.

Habari njema ni kwamba mtazamo wako binafsi na njia ya kushirikiana na wengine ulimwenguni si kanuni isiyoweza kubadilishwa. Kupitia kujielewa mwenyewe na wengine vyema, kuhoji mawazo na tabia zako, na kutafuta usaidizi pindi unapohitajika, unaweza kulinda na kuboresha taswira yako binafsi kijamii, na hivyo kujiruhusu kustawi katika ulimwengu wetu wenye jamii tete.