Blogu

Our Everyday Tasks Depend on Core Cognition

Kazi Zetu za Kila Siku hutegemea Ufahamu

Ufahamu huathiri utendakazi wako wa msingi kama vile kumbukumbu, umakini, na mwingiliano wa kila siku ulimwenguni. Kuelewa jinsi ufahamu wako unavyofanya kazi kunaweza kukusaidia kuulinda na kuuboresha.

Ikiwa umewahi kuona mtoto akijifunza ujuzi mpya, kama vile kuzungumza au kuitikia sauti, basi umeshuhudia utengenezwaji wa ufahamu, ni seti ya uwezo ambao kimsingi hutuwezesha kufanya kazi kwa kujitegemea ulimwenguni. Hujumuisha shughuli za kiakili kama vile umakini, kumbukumbu, kujifunza, na kujidhibiti.

Ufahamu ni mojawapo ya vipengele (kategoria) vidogo vinavyopimwa katika kipimo cha MHQ cha Milioni ya Afya ya Akili (Kiwango cha Afya ya Akili). Uwezo huu ndio msingi wa ujenzi wa kiwango cha juu cha utendaji kazi.

Kuwa na ufahamu wenye afya humaanisha kuwa, una uwezo wa:

  • Kuonyesha kujidhibiti katika mawazo na matendo yako
  • Kujifunza na kutekeleza stadi mpya
  • Kuunda lugha na kuwasiliana na wengine
  • Kuhifadhi taarifa muhimu kwenye kumbukumbu yako
  • Kuzingatia kazi za kimsingi na kugundua kinachoendelea karibu nawe

Vinginevyo, ikiwa una matatizo katika eneo hili, unaweza:

  • Pambana na tabia za kulazimishana
  • Usiwe na uwezo wa kupumzika au kutulia, hata pindi inapohitajika
  • Kusikia, kuona, kuhisi, kunusa au kuonja vitu ambavyo watu wengine hawavihisi (mauzauza)
  • Kuwa na nyakati za kuchanganyikiwa au kuchelewa kufikiri pindi usipoweza kuelewa mambo

Sababu za Kiwango cha Chini cha Ufahamu

Kuna sababu mbalimbali zinazoweza kuathiri kiwango cha ufahamu. Kuna hali kadhaa, kama vile ADHD, ambayo huhusisha ugumu wa kuwa makini na kuzingatia, kipengele kimoja cha ufahamu. Hali nyingine, kama vile Tatizo la Usonji (ASD), inaweza pia kuhusisha matatizo katika ufanyaji kazi wa hisia. Ukichaa pia mara nyingi huathiri kumbukumbu na utendakazi wa siku hadi siku, huku unyogovu, ugonjwa wa mfadhaiko usababishwao na janga fulani (PTSD), na ugonjwa wa kuweka mkazo kwenye mambo kupita kiasi (OCD) yote huhusishwa na dalili zinazohusiana na ufahamu. Kwa hakika, kuna hali chache sana za afya ya akili na neva zisizoathiri ufahamu kwa namna fulani.

Wakati mwingine mabadiliko makubwa zaidi au ya ghafla katika ufahamu yanaweza kusababishwa na hali ya matibabu au jeraha la ubongo. Ukikumbana na mabadiliko makali kama hayo, kama vile kuchanganyikiwa kuhusu mahali ulipo au jambo linaloendelea (au kushuhudia mabadiliko haya kwa mtu mwingine), piga simu kwa huduma za dharura zilizopo kwenye eneo lako. Hii inaweza kuwa ishara ya tahadhari ya jambo zito zaidi, na hivyo kutafuta msaada upesi kunaweza kuleta mabadiliko.

Ikiwa haujapitia mabadiliko ya ghafla hivi karibuni, lakini una alama ya chini sana ya ufahamu kwenye kipimo cha MHQ (0 au pungufu), unapaswa kufanyiwa tathmini na mtaalamu wa matibabu haraka iwezekanavyo. Mtaalamu wa tiba anaweza kukusaidia kugundua sababu inayopelekea kiwango hiko cha chini cha ufahamu na kuishughulikia.

Je, Ninaweza Kuongeza Ufahamu Wangu?

Jinsi gani na kama utaweza kuongeza alama yako ndani ya muda mfupi itategemea ni nini kinachosababisha shida hiyo. Ikiwa hapo awali umeshawahi kutibiwa tatizo la afya ya akili au suala la mfumo wa neva linaloathiri utendakazi wako wa kila siku, basi unapaswa kulishughulikia na kulidhibiti tatizo hilo kwanza. Usaidizi wa dawa na wa kitabia kutoka kwa mtaalamu wa tiba ama mtaalamu mwingine unaweza kukusaidia kupunguza dalili hizo, au ikiwezekana kurahisisha maeneo ya maisha yako yaliyo na changamoto.

Kwa mfano, ikiwa unapata taabu katika masuala ya kutumia umakini, wakati mwingine dawa zinaweza kulishughulikia hili, kama vile tu mabadiliko ya lishe na chaguzi za shughuli zinavyoweza kufanya. Daktari wa magonjwa ya akili au mtaalamu wa tiba anayefahamu changamoto hizi pia anaweza kukusaidia kurahisisha kazi za kila siku, kukusaidia kujifunza ujuzi mpya au kutafuta usaidizi wa mambo yaliyo magumu kwako. Ikiwa hauna uhakika ni wapi unaweza kupata huduma hii, unaweza kuwasiliana na Idara ya Huduma za Afya ya Akili na Udhibiti wa Matumizi Mabaya ya Dawa (SAMHSA) kama upo nchini Marekani.

Ikiwa una alama chanya ya ufahamu katika kipimo cha MHQ, kuna njia za kuiboresha hatua kwa hatua na kuilinda baada ya muda. Kwa mfano, Idara ya Afya ya Chuo cha Harvard imebainisha kuwa shughuli fulani zinazounganisha mafunzo ya kimwili na kiakili, kama vile tai chi, zinaweza kuimarisha utendaji kazi wa ubongo wako. Idara ya Afya ya Chuo cha Harvard pia imebainisha kuwa uboreshaji wa afya ya kimwili, kupitia lishe na mazoezi, unaweza kuboresha utendaji kazi wa ubongo. Unaweza pia kushirikiana na daktari wako ili kuboresha shinikizo la damu yako, sukari ya damu na kiwango cha lehemu, vitu vinavyochangia afya ya ubongo na vilivyo muhimu kwa ustawi wa kimwili na kiakili.

Pia ni wazo nzuri kuendelea kuupa changamoto chanya ubongo wako. Watu wengi wanajua kuwa shughuli kama vile mafumbo ya maneno na michezo ya hesabu zinaweza kusaidia afya ya ubongo na ufahamu. Tafuta michezo ya kiakili inayokufurahisha na inayokupatia changamoto.

Ufahamu huathiri maeneo yote maishani mwako na huweza kuathiriwa na mambo mbalimbali. Ni muhimu kufahamu alama yako ya ufahamu na kutafuta usaidizi kama ikihitajika.